Sep 26, 2021 08:08 UTC
  • 'Mhusika Mkuu' wa mauaji ya kimbari Rwanda afariki dunia nchini Mali

Kanali Théoneste Bagosora, anayehesabiwa "mhusika mkuu" wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, amefariki dunia katika hospitali moja katika mji mkuu wa Mali, Bamako.

Hiyo ni kwa mujibu mamlaka ya magereza nchini Mali. Kanali Théoneste Bagosora alikuwa akitumikia kifungo nchini Mali, baada ya kuhukumiwa na mahakama ya Umoja wa Mataifa.

Mahakama ya uhalifu wa kivita kwa ajili ya Rwanda ICTR ambayo makao yake makuu yalikuwa mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania, ilimhukumu kifungo cha maisha kanali huyo wa zamani wa kijeshi kwa mauaji ya halaiki yaliyofanyika mwaka 1994 nchini Rwanda.

Théoneste Bagosora, amefariki nchini Mali akiwa na umri wa miaka 80. Kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu Rwanda (ICTR), wakati huo alikuwa kiongozi wa juu kabisa katika jeshi nchini Rwanda baada ya shambulio dhidi ya ndege ya Rais Juvénal Habyarimana.

Watu wapatao 800,000 waliuawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda  yaliyotplea mwaka 1994 

 

Bagosora alikamatwa mnamo mwaka 1996 nchini Cameroon ambapo alihukumiwa kifungo cha maisha mnamo mwaka 2008. Miaka mitatu baadaye, mahakama ilibatilisha hukumu hiyo na kupunguza adhabu yake hadi kifungo cha miaka 35. Alikuwa akitumikia kifungo chake nchini Mali katika gereza la Koulikoro na watu wengine waliohukumiwa na ICTR huko Arusha.

Mahakama ya ICTR ilimpata na hatia ya uhalifu uliofanywa kati ya Aprili 7 na 9, 1994, pamoja na ubakaji na mauaji ya watu wengi. Kama mkuu wa majeshi, pia alihukumiwa kwa mauaji ya watu kadhaa wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Agathe Uwilingiyimanana walinda amani 10 wa Ubelgiji.

Watu wapatao 800,000 waliuawa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 pale waasi wa Kihutu wenye msimamo mkali walipowauwa Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani.