Sep 26, 2021 16:32 UTC
  • Musalia Mudavadi
    Musalia Mudavadi

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) amesema kuwa kauli ya Naibu Rais wa nchi hiyo, William Ruto ya "taifa la mahsla" inapigia debe umasikini na kwamba Kenya si nchi ya walalahoi.

Musalia Mudavadi amesema mtindo wa uchumi wa kuanzia mashinani wa Ruto unaendeleza na kutukuza umasikini kati ya watu wa Kenya.

Akizungumza katika ibada ya mazishi ya Samuel Masikonde, mfanyabiashara mashuhuri, Mudavadi amesema nchi inahitaji suluhisho la kivitendo la uchumi.

Kiongozi huyo wa chama cha Amani National Congress pia ametoa wito wa kuwepo uvumilivu wa kisiasa na kampeni za amani wakati zoezi la Uchaguzi Mkuu wa 2022 linapokaribia.

Wagombea wakuu wa urais nchi Kenya hususan, Naibu Rais William Ruto, wamebuni mbinu za kuwavutia vijana na Wakenya wa kipato cha chini wakiahidi kuwasaidia wakishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Kupitia kampeni yake ya hasla, Dkt Ruto amekuwa akiahidi kuinua hali ya kiuchumi ya Wakenya wa matabaka ya chini na amekuwa akitoa misaada kwa makundi ya wachuuzi, wanabodaboda, wauzaji mboga na makanisa.

Kwa upande wake, Dkt Ruto anasisitiza kuwa mpango wa kukuza uchumi kuanzia juu umekuwa ukitenga masikini kwa kuwa unawanyima nafasi za kustawi na serikali yake itaweka mikakati ya kujenga uchumi kuanzia chini kwa kuwawezesha vijana kupata kazi na kuimarisha mazingira ya kufanya biashara.

Sera za siasa hizo za Ruto zimekosolewa sana na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga ambaye amesema, matamshi yanayotolewa na Naibu wa Rais William Ruto yanaitia nchi katika hatari ya kugawanyika na kusababisha umwagikaji wa damu. Odinga amesema kauli za Ruto zinajenga uhasama wa matabaka kwa kuendeleza siasa za kuwatenganisha wanaodaiwa kuwa navyo na wasio navyo.

Raila Odinga

Raila pia amekemea usemi wa siasa za Ruto wa makabiliano kati ya Dynasty na Mahasla  akisema kwamba mkondo huo ‘unahatarisha  uthabiti na  amani ya Kenya'.

Ruto amepanga siasa zake za kuwania urais kwa msingi wa kuwatetea 'mahasla'  wasio nacho dhidi ya wanasiasa wanaodaiwa kuwa na mali kutoka familia tajika kisiasa. Vuguvugu la mahasla limeonekana kuipa wasiwasi serikali ya Kenyab kwani usemi huo unazidi kushika kasi na kutawala mijadala kuhusu siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao.