Sep 27, 2021 04:34 UTC
  • Wanajeshi wa SADC waua magaidi 17 kaskazini mwa Msumbiji

Jumuiya ya Maendeleo ya Kuisni mwa Afrika SADC ambayo imetuma wanajeshi wake nchini Msumbiji ili kuisaidia nchi hiyo kupambana na magaidi imesema kuwa, wanajeshi wake wameua magaidi 17 katika jimbo la Cabo Delgado baada ya kusambaratisha maficho yao huko Chitama.

Mapigano hayo yalitokea Jumamosi na kusababisha pia kifo cha mwanajeshi mmoja wa SADC na kujeruhiwa wengine watatu. Taarifa hiyo imesema kuwa wanajeshi wa SADC waliojeruhiwa kwenye mapigano hayo, wanaendelea vizuri.

Kwa muijbu wa taarifa hiyo, jana Jumapili pia, wanajeshi hao walipambana na genge jingine la kigaidi kusini mwa Mto Messalo. Gaidi mmoja aliuawa na mwingine mmoja kutiwa mbaroni.

Mwezi Julai mwaka huu, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC ilianza kutuma wanajeshi wake kulisaidia jeshi la Msumbiji kupambana na magaidi waliojizatiti kaskazini mwa nchi hiyo.

Wakimbizi wa Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji

 

Rwanda ilikuwa nchi ya kwanza kutuma wanajeshi wake 1,000 nchini Msumbiji ikifuatiwa na Botswana iliyotuma wanajeshi 296 na baadaye Afrika Kusini wanajeshi 1,500.

Zimbabwe kwa upande wake imetuma walimu 304 wa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi wa Msumbiji na kuwapa mbinu za kupambana na waasi.

Mwishoni mwa mwezi Julai, wanajeshi wa Rwanda walisema kuwa, walishapambana mara kadhaa na watu wenye silaha na kufanikiwa kuua magaidi 30 hadi wakati huo. Tarehe 8 Agosti mwaka huu, wanajeshi wa Rwanda walifanikiwa kuudhibiti mji wa bandari wa Mocimboa da Praia uliokuwa umetekwa na waasi.