Sep 27, 2021 13:00 UTC
  • Serikali ya Ethiopia yawataka waasi kujisalimisha; iko tayari kuwasamehe

Serikali ya Ethiopia imewataka wapiganaji wa makundi ya waasi nchini humo wajisalimishe na kwamba, iko tayari kutoa msamaha kwa wanachama na viongozi wa makundi hayo.

Taarifa ya serikali ya Addis Ababa imesisitiza kuwa, watakaojisalimisha na kukabidhi silaha watapatiwa msamaha na kwamba, watakuwa katika amani ya kudumu.

Msimamo huo wa Ethiopia unatolewa katika hali ambayo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yameendelea kuyalaumu mataifa ya Afrika kwa kuendelea kutoa msamaha kwa waasi ambao wamehusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Mapigano kwenye mikoa ya Tigray, Amhara na Afar nchini Ethiopia, yameripotiwa kuanza kusambaa kwenye maeneo mengine ya taifa hilo la Pembe ya Afrika huku raia wakiendelea kupoteza maisha yao.

Wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF)

 

Mapigano baina ya jeshi la taifa la Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) yalianza tokea Novemba mwaka jana, na yanaendelea mpaka sasa licha ya Addis Ababa kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja mnamo Juni 28. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, mbali na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) walipinga na kukosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika ya kumteua aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo kuwa mpatanishi katika mgogoro unaoshuhudiwa kwa miezi kadhaa sasa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.