Oct 03, 2021 12:45 UTC
  • Magaidi 19, akiwemo kamanda wa ngazi ya juu, wauawa Msumbiji

Magaidi 19, akiwemo kamanda wa ngazi ya juu wa genge moja la kigaidi, wameuawa katika operesheni ya kiusalama iliyofanywa na wananjeshi wa kieneo huko kaskazini mwa Msumbiji.

Katika taarifa, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo imetuma wanajeshi nchini Msumbiji ili kuisaidia nchi hiyo kupambana na magaidi imesema kuwa, wanajeshi wake wameua magaidi 18 akiwemo kamanda mwandamizi wa genge hilo katika jimbo la Cabo Delgado.

SADC imefafanua kuwa, Rajab Awadhi Ndanjile, kamanda mkuu wa genge moja la kigaidi ni miongoni mwa magaidi 19 waliouawa katika shambulio lililofanywa na askari wa jumuiya hiyo ya kikanda mnamo Septemba 25 katika wilaya ya Nangade mkoani Cabo Delgado.

Magaidi wenye mfungamano na ISIS nchini Msumbiji

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika imebainisha katika taarifa hiyo ya jana Jumamosi kuwa, Ndanjile amekuwa akiongoza shughuli ya kuwasajili vijana kujiunga na genge lake la kigaidi, sambamba na kuongoza mashambulizi dhidi ya vijiji vya wilaya ya Nangade na vilevile kuwateka nyara wanawake na watoto wadogo.

Mwezi Julai mwaka huu, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ilianza kutuma wanajeshi wake kulisaidia jeshi la Msumbiji kupambana na magaidi waliojizatiti kwa silaha huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags