Oct 05, 2021 02:55 UTC
  • Makumi ya askari wauawa na kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi Burkina Faso

Wanajeshi wasiopungua 14 wa serikali ya Burkina Faso wameuawa katika shambulizi la kigaidi huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Duru za kiusalama zimethibitisha habari hizo na kuongeza kuwa, wanajeshi 14 wa Burkina Faso wameuwa katika shambulizi hilo la jana Jumatatu, huku wengine saba wakijeruhiwa.

Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Aime Barthelemy Simpore amesema katika taarifa kuwa, askari hao waliuawa na kujeruhiwa baada ya genge la wanamgambo waliojizatiti kwa silaha kushambulia kambi ya jeshi ya Yirgou iliyoko katika mkoa wa Sanmatenga kaskazini mwa nchi.

Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na mauaji hayo, ingawaje wanamgambo wenye mfungamano la makundi ya kigaidi ya al Qaeda na Daesh wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini humo.

Askari wa Burkina Faso wakilinda doria

Wakazi wa mkoa huo wameshtushwa mno na mauaji hayo ya maafisa usalama, kwa kuwa hali ya usalama ilikuwa imeanza kuboreka katika eneo hilo kutokana na uwepo wa wanajeshi wa serikali kwa muda sasa.

Maelfu ya watu wameuawa katika mashambulizi ya makundi hayo kwenye nchi za Mali, Niger na Burkina Faso na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.  Tarehe 4 Juni 2021 zaidi ya watu 132 waliuliwa kwa umati katika shambulizi la magaidi katika kijiji cha Solhan mkoani Yagha, mpakani mwa Burkina Faso na Niger.

Tags