Oct 05, 2021 08:10 UTC
  • Rais wa Msumbiji ataka magaidi wajisalimishe baada ya kinara wao kuuawa

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji ametoa mwito kwa magenge ya kigaidi kusalimu amri baada ya kinara wao kuuawa hivi karibuni kaskazini mwa nchi.

Nyusi alitoa mwito huo jana Jumatatu na kueleza kuwa, magaidi hao wanapaswa kujisalimisha kwa vyombo vya usalama kwa kuwa hawana chaguo jingine wala pahala pa kutorokea.

Rais Nyusi amesema, "tunawatolea mwito wasisubiri kifo, hilo sio lengo la maafisa wa usalama na ulinzi. Jisalimishe, kwa kuwa huna pa kukimbilia, unakimbia kutoka msitu mmoja hadi mwingine na daima unakimbizwa."

Wito wa Rais wa Msumbiji unakuja siku chache baada ya magaidi 19, akiwemo kamanda wa ngazi ya juu wa genge moja la kigaidi, kuuawa katika operesheni ya kiusalama iliyofanywa na wanajeshi wa kieneo huko kaskazini mwa Msumbiji.

Magaidi wa ASJW Msumbiji

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo imetuma wanajeshi nchini Msumbiji ili kuisaidia nchi hiyo kupambana na magaidi imesema kuwa, wanajeshi wake hivi karibuni waliua magaidi 18 akiwemo Rajab Awadhi Ndanjile, kamanda mwandamizi wa genge la kigaidi la Ahlu Sunnah Wal Jama'a (ASWJ) katika wilaya ya  Nangade jimboni Cabo Delgado.

Watu zaidi ya elfu tatu wameuawa hadi sasa, huku wengine zaidi ya laki nane wakilazimika kuwa wakimbizi katika mkoa wa Cabo Delgado tokea mwaka 2017.

Tags