Oct 06, 2021 12:45 UTC
  • Askari watoto wakombolewa na wanajeshi wa Msumbiji

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema vikosi vya serikali ya Msumbiji vimefanikiwa kuwakomboa watoto waliosajiliwa kwa nguvu na kutumiwa vitani na genge la kigaidi la al-Shabaab kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Msemaji wa UNICEF, James Elder bila kueleza idadi au hali ya watoto hao waliookolewa, amewaambia waandishi wa habari mjini Vienna kuwa, "watoto wamekombolewa, wala hawajaachiliwa na magaidi. Wamekombolewa na vikosi vya serikali."

Amesema shirika hilo la kushughulikia maslahi ya watoto la Umoja wa Mataifa linashirikiana na serikali ya Msumbiji kuwapa matibabu ya kimwili na kisaikolojia watoto hao, na kuwasaidia kutangamana tena na jamii zao.

Elder ameongeza kuwa, licha ya kuripotiwa ongezeko la kutekwa watoto na kulazimishwa kujiunga na genge hilo la kigaidi katika mkoa wa Cabo Delgado, lakini hivi sasa eneo hilo la kaskazini mwa nchi linafikika kiwepesi kwa kiasi fulani, kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu.

Wanajeshi wa Msumbiji katika operesheni ya kiusalama

Watu zaidi ya 3,300 wameuawa hadi sasa, huku wengine zaidi ya laki nane wakilazimika kuwa wakimbizi katika mkoa wa Cabo Delgado tokea mwaka 2017.

Hata hivyo katika wiki za hivi karibuni, wanajeshi wa Msumbiji wakisaidiwa na askari wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamepata mafanikio makubwa katika makabiliano dhidi ya genge la kigaidi la Ahlu Sunnah Wal Jama'a (ASWJ) ambalo linafahamika kama 'al-Shabaab' na wakazi wa mkoa huo.

Tags