Oct 10, 2021 07:56 UTC
  • Mamilioni ya Watanzania wanasumbuliwa na matatizo ya akili

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni saba wenye matatizo yanayohusiana na afya ya akili. Hayo yamebainika wakati huu ambapo nchi hiyo ya Afrika Mashariki imejiunga na nchi zingine duniani hii leo kuadhimisha Siku ya Afya ya Akili.

Mambo mbalimbali yametajwa kusababisha matatizo ya afya ya akili nchini humo, huku mji mkuu Dar es Salaam ukitajwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wenye matatizo hayo. Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, miongoni mwa sababu zilizotajwa kuchochea tatizo hilo ni msongo wa mawazo, ugumu wa maisha na uchu wa kuwa na maisha bora.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa magonjwa yasiyoambukiza, Dkt Shedrack Makubi amesema sababu ya Dar es Salaam kuwa na wagonjwa wengi ni kutokana na wingi wa watu katika jiji hilo ambalo lina mkusanyiko kutoka mikoa mbalimbali.

Kadhalika mazingira na harakati za kutafuta maisha kwa wakazi wa jiji hilo, zimetajwa kuwa kichocheo cha watu wengi kujikuta kwenye matatizo hayo ya kiafya.

Kijana aliyezongwa na msongo wa mawazo

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, kufikia mwaka 2020 watu bilioni moja walikuwa wanaishi na magonjwa ya akili, na kwamba walio katika hatari zaidi ni wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 39.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Magonjwa ya Afya ya Akili ya Mirembe mkoani Dodoma, Dkt Paul Lawala amesema ugonjwa wa afya ya akili ni tatizo kubwa duniani kwani takwimu zinaonyesha watu milioni 300 duniani wanakabiliwa na tatizo la afya ya akili, ambapo wanahitaji msaada wa kisaikolojia, na waliofikia viwango vya juu wanahitaji matibabu.

Hivi karibuni, WHO ilitadharisha juu ya ongezeko la watu wanaokumbwa na matatizo ya kisaikolojia barani Afrika, kutokana na athari hasi za janga la Corona.

Tags