Oct 12, 2021 02:34 UTC
  • Algeria yayasusia na kuyawekea vikwazo mashirika 500 ya Ufaransa

Taasisi moja ya Algeria imetangaza habari ya kususiwa na kuwekewa vikwazo mashirika 500 ya Ufaransa nchini humo, ikiwa ni majibu ya Algiers kwa matamshi ya kifidhuli ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Jumuiya ya Waajiri ya Algeria ambayo ni muungano wa karibu mashirika 2,000 ya ujenzi, imetoa kauli na kutangaza kuwa, mashirika yanayoingiza bidhaa kutoka nje ya Algeria yameamua kuyasusia mashirika 500 ya Ufaransa yanayojishughulisha na kuingiza na kutoa bidhaa nchini Algeria kutokana na matamshi ya kifidhulu ya Emmanuel Macron.

Jumuiya hiyo imezishukuru asasi zote za kiuchumi za Algeria kwa kuamua kuyasusia mashirika 500 ya Ufaransa na kusema kuwa, matamshi ya kipumbavu ya rais wa Ufaransa dhidi ya Algeria ni lazima yalaaniwe na imetaka uhusiano wa kiuchumi wa Algeria na Ufaransa uangaliwe upya.

 

Hivi karibuni rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alidai kuwa, kabla ya Algeria kukoloniwa na Ufaransa, hakukuwa kabisa na taifa liitwalo Algeria.

Wakati huo huo jana Jumatatu, Rais wa Algeria alitangaza kuwa Ufaransa inapasa kusahau kwamba Algeria ni nchi iliyokoloniwa. Rais Abdelmajid Tebboune alisema kuwa Ufaransa iliwaua kwa umati na kufanya jinai chungu nzima dhidi ya Waalgeria katika  miaka 70 ya vita huko Algeria. Rais wa Algeria ameashiria namna Paris inavyopasa kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na nchi mbili hizo mwaka 1968 na kuongeza kuwa, matamshi ya rais wa ufaransa Emmanuel Macron ya kuidhalilisha Algeria yamejaa upotoshaji na chuki kwa lengo la kampeni za uchaguzi.

Rais wa Algeria amesisitiza kuwa, Ufaransa inapasa kusahau kwamba Algeria iliwahi kuwa koloni lake. 

Tags