Oct 12, 2021 08:04 UTC
  • Jeshi la Msumbiji lamuua kiongozi wa waasi wa chama kikuu cha upinzani

Kinara wa mrengo wa waasi wa Renamo, iliyokuwa harakati ya waasi na ambayo sasa ni chama kikuu cha siasa cha upinzani nchini Msumbiji ameuawa na wanajeshi wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha Msumbiji (FDS) kimetangaza habari hiyo na kueleza kuwa, Mariano Nhongo, kiongozi wa mrengo wa waasi wenye misimamo mikali wa Renamo aliuawa mapema jana Jumatatu, katika makabiliano na wanajeshi wa nchi hiyo.

Taarifa ya FDS imebainisha kuwa, Nhongo ameuawa pamoja na mpambe wake Ngau Kama, katika mkoa wa Sofala, baada ya kujri mapigano makali baina ya wapiganaji wao na wanajeshi wa Msumbiji katika msitu mmoja ulioko mkoani hapo, walikokuwa wamejificha.

Wiki iliyopita, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji alisema Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha nchi hiyo kimejaribu bila mafanikio, kumshawishi Nhongo na wapiganaji wake waweka silaha chini na kujisalimisha.

Rais wa Msumbiji (kulia) alipokutana na kiongozi wa zamani wa Renamo, Dhlakama Afonso

Ikumbwe kuwa, Agosti mwaka 2019, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na Ossufo Momade, kiongozi wa Renamo, walisaini mkataba wa amani wa kuhitimisha uhasama wa vita vya kijeshi; huku maelfu ya wapiganaji waliosalia wa Renamo wakikabidhi silaha zao kwa vyombo vya usalama.

Mnamo katikati ya muongo wa 1970, Renamo iliendesha vita vikali vya ndani dhidi ya serikali ya chama cha Frelimo vilivyosababisha vifo vya watu milioni moja kabla ya mapigano hayo kusita mwaka 1992. Mapigano mapya baina ya pande mbili yalizuka tena kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

Tags