Oct 12, 2021 08:08 UTC
  • Watu 13 wauawa katika mashambulio ya wanamgambo wa ADF huko DRC

Watu wasiopungua 13 wameuawa katika eneo la Oicha mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulio ya waasi wa Uganda wa ADF.

Kwa mujibu wa asasi za kiraia, wapiganaji wa ADF juzi Jumapili walishambulia vijiji vya Mabuo, Mangazi, Matekelambi na Matadi, magharibi mwa eneo la Oicha na kufanya mauaji hayo ya kikatili.

Duru za habari zinaarifu kuwa, wanamgambo hao wameteketeza kwa moto aghalabu ya nyumba katika kijiji cha Mabuo, mbali na kuiba pikipiki za wakazi wake.

Habari zaidi zinasema kuwa, idadi ya wanavijiji waliotoweka kufuatia mashambulio hayo ya ADF haijulikani. Hujuma hizo zimefanyika katika hali ambayo, mnamo Mei 6, Rais Felix Tshisekedi wa DRC aliiweka chini ya hali ya mzingiro mikoa ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, na Ituri.  

Ramani inayoonesha mikoa mitatu ya DRC inayosumbuliwa na vita na mauaji

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, mbali na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi. 

Tangu mwanzoni mwa mwezi wa Aprili, wakazi wa miji ya Beni na Butembo huko Kivu Kaskazini wamekuwa wakiandamana kulaani mauaji ya waasi wa ADF.

Tags