Oct 12, 2021 16:11 UTC
  • ICJ yakataa madai ya Kenya katika mzozo wa mpaka wa baharini na Somalia

Mahakama ya UN imetoa uamuzi kwa maslahi ya Somalia katika mzozo wa muda mrefu wa nchi hiyo na Kenya juu ya mpaka wa baharini wa pande hizo mbili.

Kesi hiyo ilihusu pembetatu yenye ukubwa wa kilomita mraba 38,000 katika Bahari ya Hindi ambayo inadhaniwa kuwa na utajiri wa mafuta na gesi.

Mzozo huo umekuwa kiini cha mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbilii jirani. Kenya imesema mstari unaoelekea mashariki mwa mahali ambapo nchi hizo mbili zinakutana pwani unawakilisha mpaka wa baharini.

Somalia, inapinga suala hilo ikisema kwamba mpaka wa bahari unapaswa kufuata mwelekeo sawa na mpaka wa ardhi.

Jopo la majaji 14 waliokaa The Hague nchini Uholanzi kuamua kesi hiyo limesema kwamba Kenya haijathibitisha kuwa Somalia hapo awali ilikubaliana na mpaka wake uliodaiwa.

Badala yake, majaji hao walichora laini mpya ambayo imegawanya eneo lenye mgogoro katika sehemu mbili. Hata hivyo Mahakama ya ICJ haina njia ya kutekeleza maamuzi yake.

Somalia iliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikisema mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mzozo huo yameshindwa. Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa Somalia ilikasirishwa na hatua ya Kenya kuuza leseni za uchunguzi wa raslimali za mafuta na gesi katika eneo lenye mzozo kwa mataifa mawili mnamo 2012.

Wiki iliyopita, serikali ya Kenya ilitaja kesi hiyo kuwa ni "mchakato wa mahakama wenye makosa". Iliongeza kuwa kulikuwa na "upendeleo wa asili" na kwamba korti hiyo ilikuwa njia isiyofaa ya kutatua mzozo huo.

Tags