Oct 13, 2021 12:58 UTC
  • UN: Watoto, wanawake 1,000 wanaozuiliwa Libya wapo hatarini

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) umetadharisha kuhusu hali mbaya inayowakabili watoto wadogo na wanawake wapatao elfu moja ambao ni miongoni mwa maelfu ya wahajiri wanaozuiliwa katika kambi za wakimbizi za kuogofya huko Tripoli, mji mkuu wa Libya.

Taarifa ya Unicef imeeleza kuwa, wanawake 751 na watoto 255 ni miongoni mwa maelfu ya wahajiri na wakimbizi wanaotafuta hifadhi waliokamatwa na kuzuiliwa jijini Tripoli mwezi huu.

Unicef imesema watoto wadogo watano wasio na wazazi au wasimamizi na wengine 30 ni miongoni mwa wahajiri waliokamatwa na wanahitaji msaada wa dharura.

Shirika hilo la kushughulikia watoto la Umoja wa Mataifa limeeleza bayana kuwa, wahajiri hao wanakabiliwa na masaibu na unyanyasaji unaofanywa na maafisa wa serikali na pia magenge ya wahalifu.

Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka imesema wakimbizi wasiopungua 5,000 walikatwa kwa umati na kuzuiliwa katika kambi za kutisha, mbali na kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji huko Tripoli.

Baadhi ya wahajiri wanauzwa kama watumwa huko Libya

Haya yanajiri siku chache baada ya Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kulaani mauaji ya wahajiri wasiopungua 6 waliopigwa risasi na walinzi wa kambi ya kudhibiti wahajiri haramu iliyoko ya Al-Mabani mjini Tripoli.

Msemaji wa kamisheni hiyo mjini Geneva, Marta Hurtado amesema mashaka na masaibu yanayowapata wakimbizi na wahajiri huko Libya yanatia wasiwasi mkubwa.

Tags