Oct 13, 2021 12:58 UTC
  • Kenya yapinga uamuzi wa ICJ kuhusu mzozo wa mpaka wa baharini na Somalia

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amepinga uamuzi uliotolewa jana Jumanne na Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ), kuhusu mzozo wa muda mrefu wa nchi hiyo na Somalia juu ya mpaka wa baharini wa pande hizo mbili.

Katika taarifa, Rais Kenyatta amesema ingawaje Kenya haijashangazwa na uamuzi huo wa ICJ, lakini inatiwa wasi wasi na matokeo hasi yatakayosababishwa na uamuzi huo kwa eneo zima la Pembe ya Afrika.

Rais wa Kenya amedai kuwa, katika hali ambayo nchi hiyo ya Afrika Mashariki inaheshimu utawala wa sheria, lakini inapinga vikali wala haitambui uamuzi huo wa ICJ, kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza na kutatua baadhi ya mizozo kwa mujibu wa Tangazo la Mwaka 1965.

Hapo jana, Mahakama hiyo ya UN ilitoa uamuzi kwa maslahi ya Somalia katika mzozo huo wa muda mrefu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na Kenya juu ya mpaka wa baharini wa pande hizo mbili. Eneo hilo linalozozaniwa na pande mbili na lenya ukubwa wa kilomita mraba 38,000 katika Bahari ya Hindi inadhaniwa kuwa na utajiri wa mafuta na gesi.

Majaji wa mahakama ya ICJ iliyoko Hague, Uholanzi

Somalia iliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi ikidai kuwa, mazungumzo baina yake na Kenya ya kutafuta suluhisho la mzozo huo yamegonga mwamba.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya wiki iliyopita ilisema nchi hiyo imeungana na nchi nyingine nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutika kutotambua mamlaka rasmi ya mahakama ya ICJ, mbali na kujitoa katika kesi hiyo iliyofikia tamati jana.

 

Tags