Uganda kutuma askari polisi 160 wa kulinda amani Somalia
Uganda inajiandaa kutuma maafisa wa polisi wapatao 160 nchini Somalia, kwenda kushiriki operesheni za kudumisha amani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Katika taarifa jana Alkhamisi, jeshi la polisi la Uganda limesema askari polisi hao wamekamilisha kozi ya miezi ya miezi sita, na wanatazamiwa kutumwa Somalia mwezi Disemba mwaka huu.
Taarifa ya polisi ya Uganda imeongeza kuwa, "wakiwa nchini Somalia, maafisa hao mbali na kusaidia katika kudumisha nidhamu ya umma, lakini pia watawalinda maafisa na wafanyakazi wa Umoja wa Afrika pamoja na taasisi zao."
Maafisa hao wa polisi wa Uganda wanatazamiwa kuwa sehemu ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom), ambao hutumwa nchini Somalia kwa mzunguko.

Hii itakuwa duru ya kumi kwa Uganda kutuma maafisa wake wa polisi wa kulinda amani nchini Somalia.
Amisom inaundwa na askari 22,000 kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone, pamoja na maafisa wa polisi kutoka Nigeria, Sierra Leone na Uganda.