Oct 15, 2021 06:35 UTC
  • Kiongozi wa genge la kigaidi la Daesh aangamizwa nchini Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuangamizwa kiongozi wa genge la kigaidi la Daeshi yaani ISIS kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Ufaransa limenukuu taarifa ya jeshi la Nigeria iliyotolewa jana ikisema kuwa, Abu Musab al Barnawi, mkuu wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko magharibi mwa Afrika ameuliwa na jeshi la Nigeria.

Hata hivyo hakukutolewa maelezo zaidi kuhusu namna mkuu huyo wa genge la kigaidi la Daesh Afrika Magharibi alivyouawa.

Ripoti zinasema kuwa, Abu Musab al Barnawi ambaye jina lake la asili ni Habib Yusuf alikuwa mwanachama wa genge la kigaidi la Boko Haram kabla ya kujitenga na kuwa kiongozi wa genge la Daesh huko Nigeria.

Magaidi wa ISWAP nchini Nigeria

 

Nigeria imekumbwa na mashambulio mengi ya kigaidi, ya kikatili na ya umwagaji wa damu katika miaka ya hivi karibuni. Mashambulizi hayo yalianzia kaskazini mwa nchi hiyo na baadaye kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo na hadi katika nchi jirani zinazopakana na Nigeria ambazo ni Niger, Chad na Cameroon.

Genge la Boko Haram lilijitokeza mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria kwa madai ya kupambana na kile kilichotajwa na genge hilo kuwa ni elimu za Magharibi. Kwa mujibu wa itikadi potofu za genge hilo la ukufurishaji, elimu zote linazodai ni za Magharibi, ni haramu na ndio maana ya neno Boko Haram.

Mwaka 2016 genge la Daesh (ISIS) lilijiengua kutoka kwenye genge la Boko Haram na kuanzisha genge jipya la kigaidi  lililolipachika jina la ISWAP.

Tags