Oct 16, 2021 12:04 UTC
  • WHO yaazimia kupambana na unyanyasaji wa kingono DRC

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, linatuma watalaamu ili kuzuia unyanyasaji wa kingono katika nchi 10 zenye hatari kubwa ya uovu huo, baada ya kashfa kubwa kuripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus ametangaza mipango yake ya kushughulikia tatizo hilo wakati wa kikao cha faragha na wawakilishi wa nchi 194 wanachama wa shirika hilo.

Uamuzi huo wa WHO unakuja siku chache baada ya wahudumu wa shirika hilo na wafanyakazi wengine wa utoaji misaada kukabiliwa na kashfa ya kujihusisha na vitendo vya kuwanyanyasa kingono wanawake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, tayari mtalaamu mmoja amepelekwa katika Jamhuuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini haikutaja mataifa mengine sita yanayoshuhudia kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake.

Hivi karibuni, Dakta Tedros Adhanom Gebreyesus Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) aliomba radhi baada ya kutolewa matokeo ya uchunguzi huru kuhusu hatua ya wafanyakazi wa shirika hilo kuhusika na udhalilishaji wa kijinsia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aghalabu ya wahanga wa matukio hayo walikuwa wakifanya kazi mbalimbali za kutoa huduma katika ofisi ya WHO huko DRC.

Katika miaka ya karibuni kulichapishwa ripoti nyingi kuhusu kuhusika wafanyakazi wa sekta ya afya na wale wa ndani na kimataifa wa Shirika la Afya Duniani katika kuwabaka wanawake na mabinti wa Kikongo; ambapo baada ya kamati teule kufanya uchunguzi wake imebainika wazi kuwa akthari ya ripoti hizo ni sahihi.