Oct 18, 2021 03:52 UTC
  • Wahajiri kadhaa wafariki dunia katika ajali ya boti pwani ya Algeria

Wizara ya Ulinzi ya Algeria imesema wahajiri wanne wamekufa maji baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama katika Bahari ya Mediterania, huko pwani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Taarifa iliyotolewa jana Jumapili na wizara hiyo imesema, Gadi ya Pwani ya Algeria huku ikitumia helikopta ya kijeshi imefanikiwa kuokoa wahajiri haramu 13 katika ajali hiyo, umbali wa maili 16 kaskazini mwa mji mkuu, Algiers. 

Hata hivyo taarifa hiyo ya Wizara ya Ulinzi ya Algeria haijatoa maelezo kuhusu uraia wa wahamiaji hao haramu walioaga dunia au kuokolewa kwenye ajali hiyo katika Bahari ya Mediterania.

Licha ya Algeria kupasisha sheria mwaka 2009 inayotoa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela kwa vitendo vya uhamiaji haramu, lakini hilo halijawazuia maelfu ya vijana wa Kialgeria kuhatarisha maisha yao kwenda Ulaya hususan Uhispania, kupitia safari hizo hatarishi.

Ajali za boti zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara katika Bahari ya Mediterania

Mapema mwezi huu, Shirika la Hilali Nyekundu la Libya lilitangaza habari ya kupatikana maiti 17 za wahajiri waliokufa maji baada ya boti waliokuwa wakisafiria kuzama  katika pwani ya magharibi ya nchi hiyo.

Katika wiki za hivi karibuni, wapiga mbizi na timu za waokoaji wameopoa makumi ya maiti za wahajiri waliozama baharini wakiwa katika safari hizo za kuogofya za kuelekea Ulaya, kwa tamaa ya kupata maisha mazuri.

Tags