Oct 18, 2021 08:43 UTC
  • Kushtadi na kupamba moto mgogoro wa kisiasa nchini Sudan

Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan umeshtadi na kuzidi kupamba moto kutokana na kushadidi na kuongezeka matatizo ya kiuchumi na vuta nikuvute za kisiasa katika nchi hiyo.

Kwa sababu hiyo, maelfu ya watu wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu Khartoum, wakiishutumu serikali ya mpito kuwa ndiye msababishaji wa hali mbaya ya kiuchumi na kisiasa inayoshuhudiwa na kutaka serikali hiyo ivunjwe.

Serikali ya mpito ya Sudan ilishika hatamu za utawala Agosti 2019 kufuatia maandamano ya upinzani ya wananchi yaliyopelekea kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al Bashir. Baada ya kushika hatamu za uongozi, serikali hiyo iliahidi kuwa itaboresha hali ya uchumi, itarejesha amani na usalama na kuandaa mazingira kwa ajili ya kuitishwa uchaguzi nchini humo. Hata hivyo licha ya kupita miaka miwili tangu ilipoundwa serikali hiyo, ahadi hizo hazijatekelezwa hadi sasa, kiasi kwamba hali ya migogoro kwa upande wa kisiasa na kiuchumi imezidi kuwa mbaya.

Omar al Bashir

Kwa upande wa kiuchumi, serikali ya mpito nchini Sudan si tu haijaweza kukidhi matarajio ya wananchi, lakini makali ya matatizo ya kiuchumi, yakiwemo ya ughali wa bidhaa, umasikini na ukosefu wa ajira yameshadidi na kuwa makubwa zaidi. Kwa mujibu wa ripoti, hali ya kiuchumi mashariki mwa Sudan ni mbaya mno mpaka imefika hadi, kwa muda wa mwezi mmoja sasa shughuli zote za kiuchumi katika eneo hilo zimelala. Kwa mujibu wa wakazi wa mashariki mwa Sudan, bei ya mkate katika eneo hilo imeongezeka mara saba na kila mkate mmoja unauzwa paundi 35 za Sudan.

Hayo yanajiri, wakati serikali ya mpito ya Sudan ilipokubali kufanya mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ilikuwa na matumaini kwamba, kwa kuiridhisha Marekani na waitifaki wake itaweza kunufaika na misaada ya madola hayo. Lakini hadi sasa haijatimiziwa ahadi hata moja ya msaada iliyopewa, huku hali ya kiuchumi ya Sudan ikizidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Maandamano dhidi ya serikali yameshtadi Sudan

Kuhusiana na nukta hiyo, gazeti la Ra'yul-Yaum limewanakili maafisa waandamizi wa Sudan na kuandika kuwa, Khartoum ilifikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv kwa tamaa na ahadi ya kupatiwa msaada na Marekani. Lakini hadi sasa Washington haijaipatia msaada wowote Khartoum.

Kwa upande mwingine, uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya Sudan ungali unaendelea na kuchochea zaidi tofauti na vuta nikuvute ndani ya nchi hiyo. Saudi Arabia, Imarati na baadhi ya nchi zingine za Kiarabu za eneo zina mkono wao katika siasa za ndani za Sudan, huku kila moja ikijaribu kuyatumia mazingira ya kisiasa yaliyopo ili kubadilisha hali ya mambo kwa maslahi yake sambamba na kuonyesha kuiunga mkono serikali ya mpito ili kulinda nafasi yake nchini Sudan.

Lakini mbali na serikali ya mpito Sudan kushindwa kutimiza ahadi za kisiasa na kiuchumi iizotoa, uchukuaji maamuzi nje ya mduara wa matakwa ya wananchi na vyama vya siasa, umezidisha manung'uniko na upinzani wa umma dhidi ya serikali hiyo. Sasa hivi Sudan inashuhudia mpasuko mkubwa na mfarakano unaozidi kuongezeka baina ya mirengo pinzani iliyoshika hatamu za uongozi wa nchi baada ya Al Bashir kuondolewa madarakani. Hali hii imesababisha hata vyama vyenye mfungamano na Omar Al Bashir virudi tena kwenye ulingo wa siasa za nchi hiyo.

Wasudan wa kada na matabaka tofauti wanaandamana kutaka serikali ya mpito ijiuzulu

Alaa kulli haal, Wasudani wengi wamezitafsiri hatua zilizochukuliwa na serikali ya mpito kuwa ni sawa na kupotezwa malengo makuu ya mapambano ya umma; na wanaitakidi kwuwa, kinyume na ilivyoahidi, serikali hiyo inafuata mkondo unaoielekeza kwenye udikteta. Na kwa sababu hiyo, muungano wa asasi za vibarua na wafanyakazi nchini humo umetaka kuhitimishwa ushirikishwaji wa wanajeshi katika utawala na kuelekezwa juhudi zote katika uundaji wa serikali maalumu ya kiraia.

Kwa namna hali inavyoshuhudiwa sasa hivi, mgogoro wa Sudan unatishia mchakato wa mpito kuelekea demokrasia; na kushadidi kwa tofauti kunaweza kusababisha fujo na machafuko nchini humo. Kwa mintaarafu ya hayo, mazungumzo baina ya vyama vya siasa, kupewa uzito matakwa ya wananchi, kukomeshwa uingiliaji wa madola ajinabi na mwisho kabisa kuitishwa uchaguzi haraka iwezekanavyo, ndiko kutakoweza kupoza kwa kiwango fulani fukuto la joto la mgogoro unaoendelea.../

Tags