Oct 18, 2021 10:01 UTC
  • Ahmed Ouyahia
    Ahmed Ouyahia

Mahakama ya Rufani ya Algeria imepasisha adhabu ya kifungo cha miaka 10 jela dhidi ya waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Ahmed Ouyahia baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi kwenye faili la kuzalisha na kununua magari la kampuni ya Sovac.

Mahakama hiyo ya Algeria imepasisha hukumu hiyo dhidi ya Ahmed Ouyahia kwa kuhusika na kashfa ya ufisadi katikana faili la kampuni ya Sovac mshirika wa kampuni ya kutengeneza magari ya Ujerumani ya Volkswagen. 

Mahakama hiyo pia imemhukumu kifungo cha miaka 10 jela mfanyabiashara Mourad Oulami ambaye ni mkuu wa kampuni ya Sovac, wakati ndugu yake, Haider, amehukumiwa kifungo cha miaka 5. 

Waziri wa zamani wa nishati wa Algeria, Youcef Yousf, pia amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kupatikana na hatia ya ufisadi katika kesi hiyo. 

Hukumu ya Ahmed Ouyahia na wenzake ilitolewa Oktoba mwaka 2020. 

Uamuzi huo ambao umetolewa na Korti ya Rufaa, ni wa mwisho na unapaswa kuanza kutekelezwa. 

Mwaka 2016 Sovac na kampuni ya kutengeneza magari ya Ujerumani, Volkswagen zilitia saini mkataba wenye thamani ya dola milioni 170 wa kuzalisha magari nchini Algeria.