Oct 19, 2021 13:33 UTC
  • Watoto 3 wauawa katika shambulio la anga Ethiopia

Umoja wa Mataifa umesema watoto watatu wameuawa huku mtu mmoja akijeruhiwa katika shambulio la anga lililolenga eneo la Mekelle, makao makuu ya eneo la Tigray kaskaizni mwa Ethiopia.

Maafisa wa afya wamenukuliwa na umoja huo wakisema kuwa, hujuma hiyo ya anga inayoaminika kufanywa na jeshi la Ethiopia ilifanyika jana Jumatatu.

Awali, serikali ya Ethiopia ilikuwa imekanusha kuhusika na shambulio hilo, lakini hii leo vyombo vya habari vya dola vimekiri kuwa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ndilo limelitekeleza, vikisisitiza kuwa lililenga ngome ya wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF).

Umoja wa Mataifa umesema kuwa unatiwa na wasi wasi kutokana na kushtadi mapigano katika eneo la hilo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia baina ya wanajeshi wa serikali ya Addis Ababa na wapiganaji wa TPLF.

Hivi karibuni, wanajeshi wa Ethiopia wakishirikiana na wenzao kutoka eneo la kaskazini la Amhara, walianzisha mashambulizi mapya katika eneo la Tigray, siku chache baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abiy Ahmed kuapishwa kwa ajili ya kuanza muhula mpya wa uongozi wake.

Watoto, wahanga wakuu wa mapigano yanayoendelea Tigray

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana (2020), kwa madai kuwa wapiganaji wa TPLF wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi. 

Hadi sasa mapigano hayo mbali na kuua maelfu ya watu, yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula. 

Tags