Oct 20, 2021 13:05 UTC
  • Wanaharakati Tunisia walaani uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao

Makumi ya wanaharakati nchini Tunisia wamefanya mkusanyiko katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis, kulalamikia na kulaani uingilliaji wa maajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Sambamba na kufanyika kikao cha bunge la Ulaya cha kuchunguza hali ya mambo nchini Tunisia, makumi ya wanaharakati wamekusanyika katika ukumbi wa maigizo wa Habib Bourguiba katika mji mkuu Tunis, na kutangaza upinzani wao dhidi ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Wanaharakati hao waliokuwa wakitoa nara za "uhuru wa kujitawala, heshima ya kitaifa" na "watu hawataki Wamarekani wala Wafaransa, wanapenda wawe na maisha", wamekosoa hatua za Marekani na Umoja wa Ulaya za kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.

Tayyib Bouaishah, mwanaharakati wa kisiasa wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Muqawama amesema, mkusanyiko huo wa upinzani uliofanyika jana sambamba na kikao cha bunge la Ulaya, unafikisha ujumbe wa wazi kabisa ndani na nje ya nchi kwamba uingiliaji wa maajinabi Tunisia haukubaliki.

Rais Kais Saied

Katika kikao chake cha jana, bunge la Ulaya lilijadili mazingira na hali ya ndani ya Tunisia baada ya uamuzi uliochukuliwa na rais wa nchi hiyo Kais Saied na athari zake kwa mwenendo wa kidemokrasia na kisiasa wa nchi hiyo.

Tarehe 14 ya mwezi huu wa Oktoba, bunge la Marekani pia la Kongresi lilifanya kikao cha kuchunguza na kujadili matukio yanayoendelea kujiri nchini Tunisia.

Itakumbukwa kuwa, tarehe 25 Julai mwaka huu, Rais Kais Saied wa Tunisia alimuuzulu waziri mkuu na kuivunja serikali sambamba na kusimamisha shughuli za bunge, hatua ambayo imelalamikiwa na kukosolewa vikali na vyama na makundi ya kisiasa ya nchi hiyo, kikiwemo chama cha Kiislamu cha An-Nahdhah.../