Oct 20, 2021 14:34 UTC
  • Kenya yaondoa marufuku ya kutembea usiku baada ya Corona kupungua

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameondoa marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwa ikitekelezwa tangu mwaka jana 2020.

Rais Kenyatta ametangaza hatua hiyo leo wakati alipoongoza wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki  kuadhimisha siku ya Mashujaa.

Sherehe hiyo iliyofanyikia katika jimbo la Kirinyaga, ilihudhuriwa na rais wa Malawi Lazurus Chakwera na viongozi wa upinzani nchini humo.

Wakenya wa matabaka mbali mbali walivumilia mvua na kibaridi kikali katika uwanja wa Wang'uru, ulioko katika jimbo la Kirinyaga, na kuhudhuria sherehe ya 58 ya mashujaa awali ikijulikana kuwa siku ya Kenyatta. Ni sherehe ambayo huwakumbuka waasisi wa taifa hilo waliopigana kumtimua beberu pamoja na wakenya waliofaulu katika Nyanja mbali mbali.

Akilihutubia taifa, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa, serikali yake imeweka mikakati kadhaa ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Rais Kenyatta amesema, "Ninaamuru marufuku ya taifa ya kutotoka nje ambayo imekuwepo tangu mwaka 2020 kuanzia usiku hadi alfajiri iondolewe mara moja."

Rais Uhuru Kenyatta

 

Katika kipindi cha majuma matatu yaliyopita, maambukizi ya virusi vya corona yamepungua kwa asilimia tano, huku idadi ya watu waliopata chanjo ikiongezeka na kufikia watu milioni 1.2.

Kuanzia tarehe mosi Novemba mwaka huu, serikali ya Kenya itatoa fedha za kuchochea sekta za Kilimo, Elimu na maeneo yaliyokumbwa na ukame.

Marufuku ya kutembea usiku ilikuwa imeathiri shughuli ambazo huendeshwa usiku huku biashara nyingi zikifungwa mwendo wa saa mbili. Zaidi ya baa 15,000 na vituo vya burudani vilifungwa wakati janga la Covid-19, lilipotangazwa huku watu 90,000 wakipoteza ajira.