Oct 21, 2021 02:22 UTC
  • Shambulio la tatu la anga la Ethiopia dhidi ya Tigray katika kipindi cha wiki moja

Serikali ya Ethiopia imetekeleza shambulio jingine la anga dhidi ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo, ikiwa ni shambulio la tatu katika kipindi cha wiki moja.

Ethiopia inasema kuwa, shambulizi hilo la jana Jumatano linaendeleza kampeni ya kupunguza nguvu vikosi vya wanamgambo wa Tigray katika vita vilivyodumu kwa takriban mwaka mmoja sasa.

Televisheni ya Tigray inayosimamiwa na Tigray People's Liberation Front, imesema mashambulizi yalilenga katikati mwa Mekele lakini haikutoa maelezo zaidi ya majeruhi au uharibifu.

Baadhi ya ripoti zisizo rasmi zinasema kuwa, watu kadhaa wameuawa na kkuujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo ya anga ya jeshi la Ethiopia.

Juzi Umoja wa Mataifa ulisema kuwa, watoto watatu wameuawa huku mtu mmoja akijeruhiwa katika shambulio la anga lililolenga eneo la Mekelle, makao makuu ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia.

tigray

Wakimbizi katika jimbo la Tigray

 

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana (2020), kwa madai kuwa wapiganaji wa TPLF wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.

Hadi sasa mapigano hayo mbali na kuua maelfu ya watu, yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula.

Mashirikka mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika jimbo hilo.