Oct 21, 2021 07:57 UTC
  • Wasudani watakiwa kushiriki kwa mamilioni katika maandamano ya leo Alkhamisi

Chama cha Wataalam wa Sudan kimetoa wito kwa matabaka yote ya wananchi kushiriki kikamilifu katika maandamano ya mamilioni yaliyopangwa kufanyika leo Alhamisi.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho imesisitiza udharura wa kufanyika mabadiliko ya kidemokrasia nchini humo ikisema wananchi wamechoshwa na utawala wa mtu mmoja.

Sambamba na hayo, wafuasi wa Harakati ya Uhuru na Mageuzi wameendelea kufanya mgomo mbele ya ikulu ya Rais mjini Khartoum kwa siku ya tano mfululizo wakitaka kuondoka madarakani serikali ya mpito ya nchi hiyo.  

Watu wanaoshiriki katika mgomo huo wanataka kuondolewa madarakani serikali ya mpito iliyoshika madaraka baada ya kufurumushwa madarakani dikteta wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir, kupanuliwa uhiriki wa makundi mbalimbali katika masuala ya utawala na kuheshimiwa vipengee vya rasimu ya kipindi cha mpito. Vilevile wanataka kuundwa serikali ya wataalamu.

Rais aliyeng'olewa madarakan Sudan, Omar al Bashir 

Mapema jana makundi 89 yanayojumuisha vyama, harakati, miungano na kamati za muqawama nchini Sudan yametishia kuanzisha uasi wa kiraia kwa madhumuni ya kukabiliana na mpango wa kuivunja serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Hayo yanajiri huku tofauti na vuta nikuvute kati ya wanajeshi na vyama vya siasa nchini Sudan zikiwa zimezidi kupamba moto na kuanza kusambaa hadi mitaani, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa udhaifu wa utendaji na kusababisha mgogoro unaoshuhudiwa hivi sasa wa machafuko mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ya mpito ya Sudan ilishika hatamu za utawala Agosti 2019 kufuatia maandamano ya upinzani ya wananchi yaliyopelekea kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al Bashir.