Oct 21, 2021 11:46 UTC
  • Baraza la Usalama UN lajadili usalama wa Maziwa Makuu Afrika

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika Huang Xia ameliambia Baraza la Usalama kuhusu umuhimu wa "kulinda mafanikio yaliyopatikana huku wakishughulikia kwa bidii changamoto zinazoendelea" katika eneo hilo.

Katika hotuba yake kwenye Baraza hilo Jumatano, Xia amesema Ukanda wa Maziwa Makuu umeshuhudia kuimarika kwa uhusiano wa nchi mbili na kusababisha kufufuliwa kwa mifumo ya ushirikiano katika nyanja ambalimbali ikiwa ni pamoja na usalama, biashara, miundombinu, uchukuzi, maliasili na nishati.

Mjumbe huyo amekaribisha maendeleo yaliyopatikana katika eneo la ushirikiano wa usalama kwa lengo la kupambana na vikundi vyenye silaha Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mjumbe Maalum amesema kuzinduliwa kwa kikundi cha mawasiliano na uratibu, ambacho kinatoa motisha isiyo ya kijeshi kwa vikundi vyenye silaha kupokonywa silaha zao, pia ni jambo muhimu la juhudi hizi katika ngazi ya kikanda.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika Huang Xia

Licha ya mafanikio haya, Xia amesema changamoto bado zipo. Amesema shughuli zinazoendelea za vikundi vyenye silaha bado ni tishio kubwa kwa amani na utulivu katika eneo hilo, na kuongezeka kuwa mashambulio, yakiwemo yanayofanywa na kundi la ADF mashariki mwa DRC au yale yaliyozinduliwa na RED-Tabara dhidi ya uwanja wa ndege wa Bujumbura mwezi Septemba ni mfano wa tishio hilo.

Mjumbe huyo Maalum amesema janga la COVID-19 pia, kwa kiwango fulani, limeongeza udhaifu wa kijamii na kiuchumi uliokuwepo awali. 

Kulingana na shirika la afya la Umoja wa Mataifa, ni dozi milioni 36 tu za chanjo ndizo zimetolewa hadi sasa katika ukanda huo, ambao una idadi ya watu karibu milioni 450.