Oct 22, 2021 10:04 UTC
  • Mufti wa Comoro: Uvumi kuhusu kuanzishwa uhusiano na Israel hauna msingi

Abubakr Abdallah Jamal al-Lail, Mufti wa visiwa vya Comoro amesema madai kuwa nchi hiyo ina nia ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel hayana msingi wowote.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Samaa, Abubakar Abdallah Jamal al-Lail aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake ya simu na Mahmoud al-Habashi, mshauri wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina anayeshughulikia masuala ya dini na uhusiano wa Kiislamu na kuongeza kuwa yale yanayoenezwa katika vyombo vya habari kuwa Comoro ina azma ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel hayana ukweli wowote.

Hii ni katika hali ambayo Jumatatu vyombo vya habari vya Israel vilidai kwamba viongozi wa utawala huo wameanzisha mazungumzo na viongozi wa Comoro kwa ajili ya kuwa na uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia wa pande mbili.

Visiwa vya Comoro ambavyo wakazi wake wengi ni Waislamu ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League, na ni nchi pekee ya Kiarabu inayopatikana kusini mwa bara la Afrika.

Waislamu wa Comoro

Vyombo vya habari vya utawala wa kibaguzi wa Israel vinasema Marekani iko katika mstari wa mbele wa nchi zinazofanya juhudi za kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala huo na visiwa vya Comoro.

Visiwa hivyo ambavyo vinapatikana katika bahari ya Hindi, mashariki mwa Afrika vina ukubwa wa kilomitamraba 1861 na kwa mujibu wa tawkimu za 2019 vina watu wapatao lakini nane na nusu.

Kufikia sasa juhudi za Marekani zimepelekea nchi nne za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco kukubali rasmi kuwa na uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel unaoendelea kukandamiza na kuwachinja kinyama watu wa Palestina wasio na hatia.

Mapatano hayo ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Wazayuni yamekabiliwa na upinzani na malalamiko makubwa ya ulimwengu wa Kiislamu.

Tags