Oct 22, 2021 14:43 UTC
  • Rais Samia Suluhu Hasan
    Rais Samia Suluhu Hasan

Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na Burundi katika kuimarisha ulinzi katika mipaka ya nchi hizo mbili. Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mazungumzo yake huko Chamwino Dodoma na Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye ambaye yupo nchini humo kwa ziara ya siku tatu.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara ya Rais wa Burundi nchini humo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili ikiwemo usalama na kulaani vitendo vya ugaidi.

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari, Marais wa Tanzania na Burundi kwa pamoja wamekubaliana kuhusu ujenzi wa reli na bandari ambazo zinakwenda kuimarisha uchumi wa nchi hizo mbili hasa Burundi kwa kuwa kwa kipindi kirefu ilikuwa kwenye vita, hali iliyochelewesha ukuaji wa uchumi kwa nchi hiyo. 

Kuhusu  ujenzi wa reli ya kisasa baina ya nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema: Tumeendeleza mazungumzo ya kujenga reli kutoka Uvinza nchini Tanzania hadi Gitega huko Burundi kupitia Msongati, na kilomita 160 zipo Tanzania na 80 zipo Burundi; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia ilionesha nia ya kujiunga na mradi huo kutoka Uvira, Burundi, hadi  Kindu DRC."

Januari mwaka huu, nchi hizo tatu zilisaini hati ya makubaliano na ushirikiano kuhusu mradi huo ambao lengo lake ni kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa.

Katika upande mwingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Tanzania inaungana na Jamhuri ya Burundi kulaani matukio ya kigaidi yaliyotokea tarehe 18 na 20 Septemba mwaka huu, yaliyosababisha vifo vya watu sita na wengine karibu 50 kujeruhiwa pamoja na uharibifu wa mali.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye 

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye kwa upande wake ameishukuru Tanzania kwa juhudi zake za kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na kujitolea ili kutimiza malengo ya jumuiya hiyo.

Ndayishimiye amesema Serikali ya Tanzania imeahidi kuiunga mkono nchi yake kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na katika kuziomba nchi ambazo ziliiwekea Burundi vikwazo kiuchumi, kuviondoa.

Ndayishimiye amewasili nchini Tanzania leo akiwa katika ziara ya siku tatu.

Tags