Oct 23, 2021 07:49 UTC
  • Licha ya upinzani wa makanisa, Rais wa DRC amwidhinisha Kadima kuwa mwenyekiti wa CENI

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amemuidhinisha Denis Kadima kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi CENI, licha ya upinzani wa Kanisa Katoliki na lile la Kiprotestanti ikiwa ni pamoja na vyama vya upinzani ukiwemo muungano wa Lamuka unaoongozwa na Martin Fayulu, na FCC inayoungwa mkono na rais wa zamani wa nchi hiyo Jospeh Kabila.

Akilihutubia taifa usiku wa kuamkia leo, Rais Felix Tshisekedi amethibitisha kuwa ameunga mkono uteuzi wa wajumbe 12 kati ya 15 wa ofisi ya CENI ambao watahusika na maandalizi ya uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika mnamo mwaka 2023.

Rais wa Kongo DR amesema, ana matumaini kwamba wajumbe watatu wa upinzani watateuliwa haraka ili kukamilisha ofisi hiyo ya CENI, na kwamba atamteua mtu atakayehusika na ufuatiliaji mzuri wa mchakato wa uchaguzi.

“Hii ndio fursa ya kumpongeza rais wa bunge la taifa ambaye ametoa fursa kadhaa kwa madhehebu ya kidini wanachama wa jukwaa husika wakutane ili kupata makubaliano baada ya kutoelewana kuhusu uteuzi wa mwenyekiti mpya. Kwa kuzingatia haya yote hapo juu nimeamua kutia saini hati hiyo inayowateua wanachama wapya wa tume ya uchaguzi CENI, ninawaonya sasa kuharakisha mchakato wa uchaguzi ulio huru na wazi katika muda uliopangwa kikatiba”, ameeleza Rais Tshisekedi.

Upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umepinga uteuzi wake Denis Kadima kwa kile unachosema kuwa ni mshirika wa karibu wa utawala uliopo madarakani nchini humo.

Katika hatua nyingine, chama cha Ensemble pour la Republique kinachoongozwa na Moise Katumbi kimesema, pamoja na kusikitishwa na hatua hiyo, bado kinatafakari iwapo kitakubali hatua hiyo ama la, wakati muungano wa Lamuka unaoongozwa na Martin Fayulu ukisisitizia kufanya maandamano ya mfululizo kupinga kuidhinishwa Kadima kuwa mkuu wa tume ya uchaguzi.

Hali ya sutafahamu sasa huenda ikaigubika Kongo DR, ambapo wanasiasa wa upinzani pamoja na Kanisa kwa pamoja wameona kuwa uchaguzi unaoandaliwa nchini humo mwaka 2023 upo mashakani.../

 

Tags