Oct 23, 2021 07:49 UTC
  • Askari wa Uganda kushtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi kwa kuua raia Somalia

Mpango wa Umoja wa Afrika wa kulinda amani nchini Somalia AMISOM umeshauri mahakama ya kijeshi ya Uganda iwafungulie mashtaka askari wa nchi hiyo wanaohudumu katika mpango huo, ambao wamehusishwa na mauaji ya raia nchini Somalia.

Jumatano iliyopita, timu iliyochunguza tukio la mauaji hayo ilisema, mamlaka za Uganda inapasa ziwafungulie mashtaka askari waliohusika na mauaji ya raia wa Somalia mwezi Agosti mwaka huu.

Wachunguzi wa Amisom walibaini kuwa, mnamo tarehe 10 Agosti, askari wa kikosi hicho waliohudumu katika eneo la Golweyn lililoko Lower Shabelle kusini mwa Somalia, yapata kilomita 110 kusini mwa mji mkuu Mogadishu waliua raia wasio na hatia wa nchi hiyo.  

Taarifa iliyotolewa jana na timu hiyo imesema: "Kwa masikitiko, watu saba waliouliwa walikuwa raia; na utendaji wa askari waliohusika ulikiuka kanuni za utendaji za Amisom."

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabaab

Mpango huo wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia umeongeza kuwa, unawabebesha dhima ya mauaji hayo askari hao kama ilivyoelezwa na timu ya wajumbe sita waliopewa jukumu la kufanya uchunguzi kamili wa tukio hilo.

Kufuatia uamuzi huo, serikali ya Uganda, ambayo ndiyo iliyochangia askari wake katika kikosi cha Amisom, ndiyo inayopaswa kuchukua hatua ya kuwapa adhabu askari hao waliohusika na mauaji hayo.

Taarifa ya Amisom imeongeza kuwa, mahakama hiyo ya kijeshi itasikiliza na kuendesha kesi ya askari hao huko huko nchini Somalia. 

Vyombo vya habari vya kujitegemea nchini Somalia vimeripoti simulizi za familia zinazoombeleza wapendwa wao zikieleza kwamba, watu saba waliouliwa na askari wa Uganda katika Amisom walikuwa ni wakulima wasio na hatia yoyote na si wanachama wa Al Shabab kundi lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.../

Tags