Oct 24, 2021 04:34 UTC
  • UNICEF: Machafuko ya Eswatini yanahatarisha mustakabali wa watoto

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetangaza kuwa, lina wasiwasi mkubwa na hali ya watoto nchini Eswatini kutokana na kuendelea kuzorota hali ya usalama kufuatia machafuko yanayoendelea katika nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Swaziland.

Mohamed M.Fall Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika amesema kuwa, hatua za kukabiliana na hali tete inayoendelea ni lazima kwanza ziheshimu na kulinda haki za msingi za watoto chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za mtoto.

Aidha amesema kuwa, watoto wameendelea kuwa wahanga wa  machafuko hayo, na kwamba, baadhi ya watoto  wameripotiwa kupata vilema, kuteswa na kukamatwa, hali ambayo inakwenda kinyume na uwajibikaji wa kisheria wa serikali kwa watoto na inaweza kuacha athari za kudumu au za muda mrefu za kimwili au kisaikolojia.

Maandamano ya kuupigania mageuzi na kuupinga utawala wa Mfalme Mswati III

 

Katika wiki za karibuni polisi ya Eswatini imelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji wanaopigania mageuzi na kuupinga utawala wa Mfalme Mswati III.

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu pia maandamano yalishadidi na kufanyika kila siku yakidai demokrasia huko Eswatini zamani ikiitwa Swaziland, ambapo waandamanaji walikuwa wakipaza sauti dhidi ya hali ya kiuchumi na kisiasa. Baadaye hali ya mambo ikatulia, lakini sasa maandamano hayo yameibuka tena katika siku za hivi karibuni yakiambatana na ghasia na machafuko.