Oct 24, 2021 04:36 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Mashambulio ya jeshi la Ethiopia yakwamisha shughuli za misaada Tigray

Mashambulizi ya anga ya jeshi la Ethiopia dhidi ya makao makuu ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo yamesababisha ndege ya misaada ya Umoja wa Mataifa kushindwa kutua mjini Mekelle.

Taarifa iliyotolewa na afisa mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffths imeeleza kuwa, ndege husika ililazimika kurejea mjini Addis Ababa.

Griffths amebainisha kwamba, tukio hilo linaongeza wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa wafanyakazi wenye dhima ya kutoa misaada ya kibinadamu katika kusaida raia wanaohitajia misaada hiyo katika jimbo la Tigray.

Hivi karibuni serikali ya Ethiopia ilianza kutekeleza mashambulio ya anga dhidi ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo, hali ambayo imezidi kuhatarisha usalama wa raia katika jimbo hilo.

Asasi na jumuiya mbalimbali za utoaji misaada zinakosoa mashambulio hayo zikisema kuwa, yanakwamisha shughuli za upelekaji misaada katika maeneo ya jimbo hilo ambapo kuna watu wanaohitajia misaada ya kibinadamu.

Athari za mashambuulio ya anga ya jeshi la Ethiopia katika jimbo la Tigray

 

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya eneo la Tigray Novemba mwaka jana (2020), kwa madai kuwa wapiganaji wa TPLF wamelishambulia jeshi la nchi hiyo na kuwaua askari waliokuwa wamelala na kupora zana zao za kijeshi.

Hadi sasa mapigano hayo mbali na kuua maelfu ya watu, yamewalazimisha watu karibu milioni mbili kuwa wakimbizi na wengine laki nne kukabiliwa na hali ngumu na ukosefu wa chakula.

Mashirikka mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika jimbo hilo.