Oct 24, 2021 15:13 UTC
  • Wanasheria Morocco wapinga chanjo ya lazima ya Covid-19

Muungano wa Mawakili nchini Morocco umepinga hatua ya serikali ya kuwalazimisha wananchi kupiga chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Muungano huo umetoa tangazo hilo leo Jumapili na kuongeza kuwa, unapinga vikali hatua ya serikali ya kuwataka wananci waoneshe vyeti vya kuthibitisha kuwa wamechanja katika usafiri wa umma, na vile vile kabla ya kuingia katika maeneo ya umma na binafsi.

Katika taarifa, wanasheria hao wamesema 'hali ya dharura' iliyotangazwa na serikali haipaswi kuwa sababu ya kukiuka katiba ya nchi na kulirejesha nyuma taifa hilo baada ya kupata mafanikio makubwa kwa suala ya haki za binadamu.

Mawakili zaidi ya 20,000 wamesaini waraka wa kuunga mkono kampeni ya kupinga chanjo ya lazima kwa wananchi wa Morocco, wakisisitiza kuwa chanjo hiyo inapaswa kuwa ya khiari.

Kuanzia Oktoba 12, serikali ya Rabat ilianza kutekeleza sheria ya kuwalazimisha watu kuonesha vyeti vinavyoonesha kuwa wamechanja kabla ya kuruhusiwa kuingia kwenye magari ya usafiri wa umma, mikawaha, maduka, na kumbi za michezo na starehe.

Uvaaji barakoa mjini Rabat

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, watu 14,606 wameaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini Morocco, huku kesi za maradhi hayo hatarishi zilizonakiliwa hadi sasa nchini humo zikipindukia 944,000.

Nchi nyingi duniani zikiwemo baadhi za Kiafrika kama vile Zimbabwe, zimetangaza kuwa wafanyakazi wa sekta za umma ambao hawajapiga chanjo ya Covid-19 hawataruhisiwa kuingia ofisini na hivyo hawatalipwa mishahara yao.

Tags