Oct 24, 2021 15:15 UTC
  • Rais wa Uganda: Mlipuko wa bomu Kampala lilikuwa shambulio la kigaidi

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema mlipuko wa bomu uliotokea usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu Kampala huenda lilikuwa shambulio la kigaidi.

Rais Museveni amesema hayo leo Jumapili katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa, "inaelekea kilikuwa kitendo cha kigaidi, lakini tutawatia mbaroni wahusika."

Museveni amebainisha kuwa, maafisa wataalamu wa polisi ya Uganda wanachunguza tukio hilo, na watatoa taarifa zaidi hapo baadaye.

Aidha amesema maafisa hao watatangaza miongozo ya kufuatwa na umma kuhusu namna ya kukabiliana na mashambulio tarajiwa ya kigaidi, akisisitiza kuwa taifa hilo litatoa kipigo kwa wahusika wa jinai hiyo.

Askari polisi wa Uganda

Ameeleza bayana kuwa, "umma usihofu, tutazima uhalifu huu kama tulivyozima vitendo vingine vya aina hii, vilivyofanywa na nguruwe wasioheshimu maisha."

Watu wasiopungua watatu wanahofiwa kuaga dunia na karibu saba wamejeruhiwa vibaya katika mlipuko huo wa bomu uliotokea usiku wa kuamkia leo katika eneo ya Komamboga Jijini Kampala kwenye eneo la kuuzia nguruwe, Tarafa ya Kawempe.

Tags