Oct 25, 2021 08:14 UTC
  • Vikosi vya jeshi vyamtia mbaroni Waziri Mkuu wa Sudan na mawaziri kadhaa

Duru za serikali ya Sudan mapema leo asubuhi zimetangaza kuwa mawaziri kadhaa na viongozi wa chama wenye mfungamano na serikali wametiwa mbaroni.

Vikosi vya jeshi vimewatia mbaroni wawakilishi wa kiraia wa baraza la uongozi wa mpito la Sudan na mawaziri kadhaa wa serikali ya mpito ya nchi hiyo. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya habari ya Sudan.  

Televisheni ya al Hadath ya Sudan imeripoti kuwa, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abdallah Hamdok pia amewekwa chini ya kifungo cha nyumbani na kuwekwa chini ya ulinzi baada ya vikosi vya jeshi visivyojulikana kuizingira nyumba yake jana Jumapili. Ripoti za vyombo vya habari na picha zinazoendelea kusambazwa mitandaoni zinawaonyesha wanajeshi wakiwa katika sare nje ya makazi ya Waziri Mkuu. 

Wakati huo huo uwanja wa ndege wa Khartoum umezingirwa na huduma za intaneti zimekatwa. Jumuiya ya Wataalamu ya Sudan (The Sudanes Professionals Association) imewatolea wito wananchi kuandamana mitaani kuzima jaribio hilo la mapinduzi. Jumuiya hiyo imesema inawahimiza wananchi kuandamana kwa wingi mitaani, waweke vizuizi barabarani na kufanya mgomo wa kutokwenda kazini ili kukabiliana na jaribio hilo la mapinduzi. 

Katika upande mwingine, Chama cha Kikomonisti cha Sudan kimesema kuwa hayo ni mapinduzi kamili ya kijeshi yaliyochochewa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan Mkuu wa Baraza la utawala la Sudan. Mwezi uliopita pia Sudan ilikumbwa na jaribio jingine la mapinduzi lililofeli. 

Jenerali  Abdul Fattah al Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan