Oct 26, 2021 04:34 UTC
  • Ghasia zashtadi Sudan, 7 wauawa huku 140 wakijeruhiwa; AU, UN na EU zatoa kauli

Kwa akali watu saba wameuawa huku wengine zaidi ya 140 wakijeruhiwa katika makabiliano baina ya waandamanaji na maafisa usalama nchini Sudan.

Maandamano hayo yalianza baada ya jeshi la Sudan kuvunja serikali ya mpito iliyokuwa inajumuisha raia na wanajeshi na wakati huo huo kuwakamata viongozi wa kisiasa akiwemo Waziri Mkuu, sanjari na kutangaza hali ya hatari nchi nzima.

Kufuatia uamuzi huo wa jeshi, waandamanaji wenye hasira walimiminika kwenye barabara za mji mkuu, Khartoum na kuwasha matairi barabarani huku milio ya risasi ikiendelea kusikika katika jiji hilo.

Jenerali Abdel Fattah Burhan, ambaye alikuwa akiongoza baraza la pamoja na viongozi wa kiraia, ametoa tangaza hilo na kusema mapinduzi ya sasa ya kijeshi yamesbabaishwa na malumbano ya kisiasa.

Amedai kuwa jeshi limelazimika kulinda usalama wa nchi kwa mujibu wa katiba na kuongeza kuwa mbali na serikali ya mpito kuvunjwa  magavana wote wa majimbo nao wamefutwa kazi na kwamba uchaguzi utafanyika Julai 2023.

Wananchi wa Sudan wakiandamana

Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kuendelea mazungumzo mara moja ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaoikabili Sudan. Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU ametaka mazungumzo baina ya raia na jeshi nchini humo yaendelee katika fremu ya tangazo la kisiasa na dikrii ya katiba.

Wakati huohuo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani 'mapinduzi ya kijeshi' yanayoendelea nchini Sudan hivi sasa, ametoa mwito wa kuachiwa huru mara moja viongozi wa kisiasa akiwemo Waziri Mkuu, Abdullah Hamdok, waliokamatwa baada ya jeshi kuvunja serikali ya mpito.

Jenerali Abdel Fattah Burhan

Kadhalika Umoja wa Ulaya kupitia Mkuu wa Sera za Kigeni wa umoja huo umetaka viongozi hao waachiwe huru haraka iwezekanavyo, huku ukilitaka jeshi liheshimu haki ya wananchi wa Sudan ya kuandamana kwa amani.

Ripoti zimebaini kuwa mawasiliano ya mtandao yamekatwa na kwamba jeshi na vikosi vya kijeshi vimepelekwa kote jijini Khartoum. Aidha uwanja wa ndege wa Khartoum sasa umefungwa, na safari za ndege za kimataifa zimesimamishwa.

Tags