Oct 26, 2021 08:08 UTC
  • Shambulio jipya la bomu laua na kujeruhi watu kadhaa nchini Uganda

Mtu mmoja ameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika mlipuko mwingine uliolenga basi la abiria nchini Uganda.

Polisi ya Uganda imethibitisha habari hiyo na kubainisha kuwa, mlipuko huo ulitokea jana Jumatatu katika wilaya ya Mpigi, katikati mwa nchi. Msemaji wa Polisi ya Uganda, Fred Enanga amesema wataalamu wa mabomu wametumwa katika eneo la Lungala, katika barabara kuu ya Kampala-Masaka, palipojiri mlipuko huo.

Amesema basi hilo la abiria lililokuwa likitokea Kampala likielekea Bushenyi, lilishambuliwa jana jioni, na kwamba mtu mmoja amethibitishwa kuuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Awali duru za habari zilikuwa zimetangaza kuwa waliouawa katika mlipuko huo ni watu wawili. 

Haya yanajiri saa chache baada ya kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) lenye itikadi za Kiwahabi kutangaza kuwa, wanachama wake ndio waliohusika na shambulio la mlipuko wa bomu katika mji mkuu wa Uganda Kampala siku ya Jumamosi, ambapo watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa.

Askari polisi wa Uganda

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda amelaani mashambulio hayo na kusisitiza kwamba, vikosi vya usalama vya nchi hiyo vitawasaka na kuwashughulikia wale waliohusika na hujuma hizo mbili anazozitaja kuwa ugaidi wa ndani.

Katika ujumbe kwenye Twitter, Museveni amesema, "viashiria vipo wazi na ni vingi, polisi inachunguza kubaini iwapo waliohusika na shambulizi la Komamboga ndio waliohusika na la jana."

Tags