Oct 26, 2021 12:12 UTC
  • Bunge la Algeria lataka matumizi ya lugha ya Kifaransa yafutwe rasmi nchini humo

Bunge la Algeria limejibu uingiliaji wa mara kwa mara wa rais na bunge la Ufaransa katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuitaka Algiers ichukue hatua za kivitendo za kufuta rasmi matumizi la lugha ya Kifaransa nchini Algeria.

Kwa mujibu wa televisheni ya "El Djazairia One" bunge la Algeria limemtaka Rais Abdelmadjid Tebboune wa nchi hiyo atoe amri ya kiserikali ya kufutwa lugha ya Kifaransa na kupiga marufuku matumizi ya lugha hiyo katika maeneo rasmi la Algeria.

Wabunge wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wamefikia uamuzi huo baada ya bunge la Ufaransa kuendelea kuidhalilisha na kuivunjia heshima mara kwa mara Algeria.

Katikati ya mwezi huu wa Oktoba pia, Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria alisema kuwa Ufaransa iliwaua kwa umati na kufanya jinai chungu nzima dhidi ya Waalegria katika  miaka 70 na kwamba Algeria si koloni tena la Ufaransa. 

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria

 

Vile vile aliashiria namna Paris inavyopasa kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na nchi mbili hizo mwaka 1968 na kuongeza kuwa, matamshi ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ya kuidhalilisha Algeria yamejaa upotoshaji na chuki na lengo lake hasa kujaribu kujinufaisha binafsi katika kampeni za uchaguzi.

Tarehe 12 mwezi huu wa Oktoba pia, Algeria ilitangaza habari ya kususiwa na kuwekewa vikwazo mashirika 500 ya Ufaransa nchini humo, ikiwa ni majibu ya Algiers kwa matamshi ya kifidhuli ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Wiki iliyopita pia, Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria alisisitiza kuwa, nchi yake itayashughulikia mafaili yanayohusiana na ukoloni wa Ufaransa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika bila ya kufumbia macho au kulegeza kamba na kwamba, katu Algiers haitafumbia macho haki yake.