Oct 26, 2021 12:18 UTC
  • Magaidi waua Waislamu 18 msikitini nchini Nigeria

Maafisa wa polisi nchini Nigeria wametangaza habari ya kuuawa Waislamu 18 waliokuwa wanasali Msikitini huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari lka Associated Press, mauaji hayo yametokea katika kijiji cha Mazakuka cha jimbo la Niger nchini Nigeria. Magaidi waliofanya unyama huo wanakisiwa kuwa ni kutoka kabila la Fulani.

Mashambulio kama hayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria. Mwaka huu mamia ya watu wameshauawa kutokana na ugomvi wa miongo mingi wa kugombania maeneo ya kilimo, maji na malisho kwenye maeneo hayo. Ugomvi mkubwa ni baina ya kabila la wafugaji la Fulani na la wakulima la Hausa. 

Mkuu wa serikali ya eneo la Mashegu, Alhassan Isah ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba watu wenye silaha waliuzingira msikiti waliokuwemo Waislamu hao wakati wa  Sala ya Alfajiri na kumimina risasi ovyo. Amesema, mbali na kuuawa Waislamu 18, Waislamu wengine wasiopungua wanne wamejeruhiwa kwenye jinai hiyo.

Jimbo la Niger, kaskazini mwa Nigeria

 

Monday Kuryas, kamishna wa jeshi la polisi la jimbo hilo la Niger la kaskazini mwa Nigeria amethibitisha kutokea jinai hiyo na kusema kuwa imetokana na ugomvi baina ya wafugaji wa kabila la Fulani na wakulima wa Hausa. 

Jinai hiyo ni mfano mwingine wa kukosekana usalama katika majimbo mengi ya Nigeria ya kaskazini magharibi na katikati mwa nchi hiyo. 

Kijiji cha Mazakuka ni kijiji cha ndani kabisa huko Nigeria. Kiko karibu kilomita 270 kutoka makao makuu ya jimbo la Niger, Minna. Mara nyingi maeneo kama hayo yanakuwa vigumu kufikiwa na maafisa wa kulinda usalama wa raia.