Oct 27, 2021 06:38 UTC
  • Kuendelea mgogoro nchini Sudan baada ya kutozaa matunda kikao cha Baraza la Usalama

Mgogoro wa kisiasa wa Sudan umezidi kuwa mkubwa baada ya majenerali wa kijeshi kufanya mapinduzi nchini humo. Maandamano ya wananchi yanaendelea huku ukandamizaji wa jeshi dhidi ya waandamanaji ukisababisha mauaji ya zaidi ya watu saba na wengine zaidi ya 140 kujeruhiwa.

Hayo yameripotiwa katika hali ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao maalumu kuhusu Sudan huku mjumbe maalumu ya umoja huo katika masuala ya nchi hiyo akitoa mwito wa mazungumzo ya amani baina ya pande hasimu nchini Sudan. Pamoja na hayo pande hizo zimeshindwa kufikia mapatano.

Machafuko nchini Sudan yalipamba moto juzi Jumatatu tarehe 25 Oktoba baada ya majenerali wa kijeshi kufanya mapinduzi yaliyoing'oa madarakani serikali ya mpito ambayo kuundwa kwake kulituliza hali ya mambo nchini humo baada ya maandamano makubwa ya wananchi yaliyopelekea kupinduliwa serikali ya Jenerali Omar al Bashir. Jenerali Abdel Fattah al Burhan aliyekuwa anaongoza serikali ya mpito iliyokuwa imeundwa na wanajeshi na raia, alitangaza siku hiyo ya Jumatatu kuwa serikali ya mpito imevunjwa na Waziri Mkuu Abdallah Hamdok alikamatwa na kuwekwa kwenye kifungo cha nyumbani katika nyumba ya Jenerali Abdel Fattah al Burhan mwenyewe kabla ya kuachiliwa huru na kurejea nyumbani. Si hayo tu, lakini pia Jenerali Abdel Fattah al Burhan ametangaza hali ya hatari katika maeneo yote ya Sudan akidai kuwa ataunda baraza jipya la uongozi litakaloendesha serikali na kusimamia uchaguzi mwaka 2023. Hii ni katika hali ambayo, kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa leo Jumatano kwa ajili ya kujadili matukio ya hivi karibuni nchini Sudan baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi, kimemalizika bila ya kutolewa taariifa ya pamoja baina ya nchi wanachama.

Maandamano nchini Sudan

 

Mgogoro nchini Sudan umeanza muda mrefu nyuma. Siasa mbovu za viongozi wa nchi hiyo ndiyo sababu kubwa ya kuongezeka mgogoro na machafuko nchini humo. Kabla ya kupinduliwa kutokana na maandamano makubwa ya wananchi, rais wa zamani wa Sudan, Jenerali Omara al Bashir alifuata siasa za kivamizi, za kichokozi na za kujipendekeza kwa mabeberu na  vibaraka wao, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uvamizi wa Yemen huku akishindwa kukabiliana na mfumuko wa bei, umasikini wa kuchupa mipaka na ukosefu wa usalama ndani ya Sudan kwenyewe. Mgogoro wa ndani ulipozidi kuwa mkubwa, wananchi wa Sudan walishindwa kuvumilia, hivyo walimiminika barabarani katika miji na mikoa yote ya Sudan kushinikiza serikali ya al Bashir ing'oke madarakani. Wanajeshi wa nchi hiyo walitumia fursa hiyo kufanya mapinduzi dhidi ya al Bashir na kuahidi kuboresha hali ya mambo ya wananchi. Hata hivyo, majenerali wa kijeshi akiwemo Abdel Fattah al Burhan mwenyewe si tu wameshindwa kushughulikia vilio vya wananchi, lakini pia wamechukua hatua za kuwakasirisha wananchi Waislamu wa Sudan kama kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na hivi sasa wanakandamiza maandamano ya amani ya wananchi.

Maandamano ya wananchi wa Sudan yaliendelea hata baada ya wanajeshi kumpindua Omar al Bashir, na hivyo wakalazimisha kuundwa serikali ya mpito yenye wawakilishi wa wananchi ili kutuliza hali ya mambo. Serikali hiyo mpya iliahidi kuendesha vizuri nchi hadi wakati wa uchaguzi. Lakini miaka miwili imepita na serikali hiyo imeshindwa kuboresha hali ya kimaisha ya wananchi. Si hayo tu lakini kama tulivyosema, serikali hiyo imejikubalisha kuwa kibaraka wa Marekani na utawala wa Kizayuni na inawafuata kibubusa vibaraka wa mabeberu kama vile Saudi Arabia kwa ahadi chapwa za kupewa misaada ya kuiwezesha kutatua matatizo yake makubwa ya ndani. 

Rais wa zamani wa Sudan, Jeneral Omar al Bashir akiwa jela baada ya kupinduliwa

 

Licha ya serikali ya mpito ya Sudan kupewa ahadi chungu nzima na madola ya kibeberu na vibaraka wao, lakini hakuna ahadi hata moja iliyotekelezwa. Gazeti la Rai al Yaum limewanukuu viongozi wa ngazi za juu wa Sudan wakisema kuwa, wakati Khartoum ilipokubali kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel, Marekani iliiahidi Sudan kuwa itaipa misaada ya kila namna, lakini hadi hivi sasa hakuna msaada wowote uliotolewa, bali hata msaada wa dola milioni 700 ulioahidiwa na Marekani kwa Sudan, nao umesimamishwa.

Kiujumla ni kwamba, wananchi wa Sudan hawaridhishwi na kuweko majenerali wa kijeshi ndani ya serikali. Lakini majenerali hao wanazidi kufanya ukaidi na wananonesha wazi kuwa hawako tayari kabisa kukabidhi madaraka kwa raia. 

Ukweli wa mambo ni kwamba hali ya Sudan ni tata na mustakbali wake haujulikani. Hivi sasa nchi hiyo imegeuzwa kuwa mwanasesere mikonoi mwa madola ya nje. Ni wazi kuwa kama mgogoro wa ndani hautatuliwa kwa njia ya mazungumzo, basi kuna hatari ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuzidi kupata nguvu uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan.

Tags