Oct 27, 2021 08:08 UTC
  • SADC yataka Zimbabwe iondolewe vikwazo vyote bila masharti yoyote

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imetoa mwito wa kuondolewa haraka na bila masharti yoyote vikwazo dhidi ya serikali ya Zimbabwe.

Taarifa iliyotolewa na Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC yenye mataifa wanachama 16 wa nchi za kusini mwa Afrika imesema, ingependa kuona hatua hiyo ikichukuliwa kwa haraka.

Sisi kama Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)  tuna wasiwasi kuhusu vikwazo vinavyoendelea kwa watu binafsi na makampuni nchini Zimbabwe," amesema Rais Chakwera wa Malawi.

Kadhalika Rais huyo ameeleza kuwa, vikwazo hivyo vya muda mrefu vimeikwamisha Zimbabwe kuboresha uchumi wake, usalama wa binadamu na ustawi endelevu.

Maandamano ya wananchi wa Zimbabwe ya kutaka nchi yao iondolewe vikwazo

Zimbabwe imekuwa chini ya vikwazo vya kiuchumi kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya EU, vikilenga watu maalumu na makampuni, jambo ambalo serikali ya Harare inalaumu kuwa ni sababu ya matatizo ya kiuchumi nchini humo.

Taarifa ya SADC imesema Zimbabwe na SADC waliweka nia ya dhati kuzungumza na wadau wakuu kuhusu kuimarisha demokrasia, utawala ha haki za binadamu.

Huko nyuma pia jumuiya kama Umoja wa Afrika na nyingine zimewahi kutoa wito wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Zimbabwse, ingawa hadi sasa madola husika hayajatekeleza matakwa hayo.

Vikwazo hivyo vilivyowekwa mwaka 2002 na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya, ambavyo ni pamoja na vizuizi vya kibiashara na kifedha, vinakadiriwa kuigharImu Zimbabwe karibu dola bilioni 100 za Kimarekani