Oct 27, 2021 08:11 UTC
  • Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kuhusu Sudan chamalizika bila natija

Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili matukio ya hivi karibuni nchini Sudan baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi, kimemalizika bila ya kutolewa taarifa ya pamoja ya nchi wanachama.

Baadhi ya wanadiplomasia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, mazungumzo ya wanachama wa Baraza la Usalama yanaendelea ili kuhakkikisha kuwa, kunafikiwa natija na kutolewa taarifa ya pamoja kuhusiana na matukio ya hivi sasa nchini Sudan.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jenerali Abdel Fattah al Burhan, Kiongozi wa mapinduzi Sudan, amesema kuwa, jeshi liliamua kuchukua mamlaka siku ya Jumatatu ili kuzuia "vita vya wenyewe kwa wenyewe". 

Wakati huo huo, taarifa zinasema kuwa, Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok alirejeshwa nyumbani kwake jana usiku, baada ya mashinikizo makubwa ya kimataifa kufuatia kuondolewa kwake katika mapinduzi ya kijeshi.

 

Jenerali Abdel Fattah al Burhan Kiongozi wa mapinduzi Sudan amebainisha kwamba, kwamba, jeshi lililizamika kuingilia kati ili kutatua mgogoro wa kisiasa uliokuwa ukiongezeka, ambao amedai, ungeweza kusababisha vita vya ndani.

Machafuko nchini Sudan yalipamba moto juzi Jumatatu tarehe 25 Oktoba baada ya majenerali wa kijeshi kufanya mapinduzi yaliyoing'oa madarakani serikali ya mpito ambayo kuundwa kwake kulituliza hali ya mambo nchini humo baada ya maandamano makubwa ya wananchi yaliyopelekea kupinduliwa serikali ya Jenerali Omar al Bashir.

Mgogoro nchini Sudan umeanza muda mrefu nyuma. Siasa mbovu za viongozi wa nchi hiyo ndiyo sababu kubwa ya kuongezeka mgogoro na machafuko nchini humo.