Oct 27, 2021 08:51 UTC
  • Rais wa Burundi autaka Umoja wa Mataifa uishirikishe zaidi nchi yake katika kusimamia amani

Serikali ya Burundi imesisitiza ushiriki zaidi wa wanajeshi wake katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Sisitizo hilo la Burundi limetolewa katika mazungumzo ya viongozi wa nchi hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anayeshughulikia masuala ya ulinzi wa amani Jean-Pierre Lacroix, ambaye yuko Bujumbura tangu Jumatatu, hii ikiwa ni ziara ya kwanza kwa afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi tangu mwaka 2016.

Jean-Pierre Lacroix amezungumza na maafisa wakuu wa nchi hiyo akiwemo rais wa nchi hiyo Evariste Ndayishimiye . Katika ajenda ya ziara hii, ilipangwa hasa kujadili masuala ya kikanda. Lakini pia ilikuwa fursa mwafaka kwa viongozi wote wa juu zaidi wa Burundi kuleta mezani suala la ushiriki mkubwa wa Burundi katika operesheni za amani za Umoja wa Mataifa.

Kwa uhakika, tangu mwaka 2020 Umoja wa Mataifa umekiondoa kikosi cha Gabon kutoka katika ujumbe wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, na wakati huo huo uliamua kuongeza idadi ya walinda amani wa ziada wa MINUSCA hadi 3,000.

Wanajeshi wa Burundi wakiwa Somalia katika kikosi cha AMISOM

 

Tangu wakati huo, serikali ya Burundi, ambayo tayari ina kikosi cha wanajeshi 750 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, imejitolea kutuma kikosi cha pili kwenye operesheni hii. Gitega pia inaomba kushirikishwa kwa upande wa MINUSMA, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, kulingana na ujumbe wa Twitter wa Jumanne hii ulioandikwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Burundi

Serikali ya Burundi imekuwa ikiingiza p[ato la fedha za kigeni kupitria kutuma askari wa kulinda amani katika maeneo mbalimbali ya operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. Inaelezwa kuwa, Burundi inaingiza zaidi ya dola milioni 20 kwa mwezi kupitia ushiriki wake katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.