Oct 27, 2021 13:32 UTC
  • Umoja wa Afrika wasimamisha uwanachama wa Sudan kufuatia mapinduzi ya kijeshi

Umoja wa Afrika umesema, umesimamisha shughuli zote za Sudan katika umoja huo baada ya jeshi kuiangusha serikali ya kiraia inayoongoza nchi hiyo.

Katika taarifa, taasisi hiyo kuu ya Afrika imesisitiza kuwa, kusimamishwa huko uwanachama wa Sudan kutaendelea hadi zitakapochukuliwa hatua athirifu za kurejesha mamlaka ya mpito ya kiraia itakayoongoza nchi kuelekea chaguzi za kidemokrasia.

Hatua hiyo ya Umoja wa Afrika imechukuliwa huku Sudan ikiwa imegubikwa na vuguvugu la uasi na migomo ya kitaifa, lililochochewa na muungano mkuu wa upinzani wa Vikosi vya Uhuru na Mabadiliko, unaolitaka jeshi liachie ngazi baada ya kunyakua madaraka ya nchi. Hayo yanajiri huku wafanyakazi wa kampuni ya mafuta ya taifa na madaktari wakijitokeza leo kujiunga na vuvuguvugu hilo la upinzani.

Jenerali wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan siku ya Jumatatu alitangaza hali ya hatari nchini kote na kuivunja serikali ya mpito pamoja na Baraza la Utawala linaloongozwa kwa ushirikiano wa jeshi na raia, likiwa na jukumu la kusimamia uendeshaji nchi hadi utakapoitishwa uchaguzi nchini humo.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

Makumi ya maelfu ya waungaji mkono wa demokrasia walimiminika mabarabarani siku ya Jumatatu katika mji mkuu Khartoum na mwingine mkubwa wa Omdurman kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyosambaratisha mchakato uliokuwa ukilegalega wa kuiongoza Sudan kuelekea demokrasia tangu lilipoibuka vuguvugu la umma mwaka 2019 ambalo lilihitimisha utawala wa muda mrefu wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir.

Kamati za wananchi katika viunga vya mji wa Khartoum zimetangaza leo kuwa zinapanga kuongoza maandamano ya upinzanin siku ya Jumamosi ambayo yameelezewa kuwa ni "maandamano ya mamilioni".

Akihutubia jana kwa njia ya televisheni, Jenerali Abdel Fattah al Burhan alisema, jeshi lililizamika kuingilia kati ili kutatua mgogoro wa kisiasa uliokuwa ukiongezeka, ambao amedai, ungeweza kusababisha vita vya ndani.

Hata hivyo mapinduzi hayo ya kijeshi nchini Sudan yamejiri ukiwa umesalia chini ya mwezi mmoja tu kabla ya muda aliopaswa Jenerali al Burhan kukabidhi uongozi wa Baraza la Utawala linaloendesha nchi, kwa viongozi wa kiraia, hatua ambayo ingelipunguza nguvu za jeshi za kushikilia madaraka.../