Oct 29, 2021 10:07 UTC
  • Wabunge Uganda watakiwa kuonesha cheti cha corona kabla ya kuingia bungeni

Naibu Spika wa Bunge la Uganda Anitah Among amewaelekeza wabunge kuwasilisha vyeti vya chanjo ya COVID-19 kabla ya kuingia bungeni.

Agizo hilo la kuwashurutisha wabunge kuwasilisha kadi zao za chanjo ya corona wanapoingia bungeni, linatarajiwa kutekelezwa kuanzia wiki ijayo. Hatua hiyo inalenga kuwahimiza Waganda kupokea chanjo kwa kuwapa mfano mzuri kupitia wabunge wao.

"Kuanzia wiki ijayo, wabunge wote wanatakikana kuwasilisha cheti chao cha chanjo ya COVID-19 watakapoingia bungeni. Lazima tuwaonyeshe wananchi kwamba, sisi ni mfano mzuri kote nchini," amesisitzia Naibu Spika wa Bunge la Uganda, Anitah Among.

Wabunge hao ni miongoni mwa Waganda wa kwanza kupokea awamu ya kwanza na ya pili ya chanjo hiyo ya COVID-19. Naibu spika huyo amewataka wabunge hao kuzidi kuzingatia kanunu za kudhibiti ugonjwa huo kwa sababu eneo la Afrika Mashariki lingali linarekodi visa vya maambukizi ya virusi hivyo.

Kwa mujibu wa Mfuko wa Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, Uganda ndiyo nchi pekee ya Afrika ambako shule bado zimeendelea kufungwa kama moja ya njia za kupunguza maambukizo ya virusi vya corona vinavyoaisumbua dunia kwa sasa.

Tags