Nov 06, 2021 03:24 UTC
  • AU yasikitishwa na shambulio la kigaidi lililoua watu 69 Niger

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani shambulio la kigaidi lililoua makumi ya watu huko kusini magharibi mwa Niger.

Katika taarifa ya jana Ijumaa, Moussa Faki Mahamat amesema AU inalaani kwa nguvu zote shambulio hilo la kigaidi lililoua watu karibu 70 wasio na hatia katika eneo la Tillabery, kusini magharibi mwa Niger.

Taarifa hiyo ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU imesisitiza kuwa, shambulizi hilo jipya la kushtua dhidi ya raia nchini Niger ni ukumbusho wa kuwepo udharura wa kuungwa mkono serikali na watu wa nchi za eneo la Sahel, katika vita dhidi ya ugaidi. 

Taarifa iliyotolewa Alkhamisi na serikali ya Niger imesema, mnamo siku ya Jumanne, watu wenye silaha waliuzingira na kuushambulia msafara wa meya wa mji wa Banibangou katika eneo lililoko umbali wa kilomita 50 kutoka mji huo katika mkoa wa magharibi wa Tillaberi karibu na mpaka wa Mali.

Watu wasiopungua 69, akiwemo meya wa mji, waliuawa katika shambulio hilo lililofanywa na watu wenye silaha kusini magharibi mwa nchi hiyo, huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Niger imetangaza siku mbili za kuomboleza mauaji hayo kuanzia jana Ijumaa. Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ya umwagaji damu, lakini duru za kiusalama zimedokeza kuwa, yumkini imetekelezwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu katika Sahara Kubwa Zaidi (ISGS).

Tags