Nov 09, 2021 12:37 UTC
  • Rosemary DiCarlo
    Rosemary DiCarlo

Mkuu wa Idara ya Siasa ya Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo amesema hatari ya Ethiopia kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ni kubwa mno", akiongeza kuwa athari za kisiasa za kushadidi ghasia nchini humo zitazidisha migogoro inayolisumbua eneo la Pembe ya Afrika.

Akihutubia Baraza la Usalama, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa na amani amesema, licha ya uvumi mwingi kuhusu jinsi mgogoro wa Ethiopia utakavyokuwa katika wiki zijazo, lakini ukweli ni kuwa hakuna mtu anayeweza kutabiri nini kitasababishwa na mapigano na ukosefu wa usalama katika nchi hiyo yenye zaidi ya watu milioni 110, zaidi ya makabila 90 tofauti na lugha 80.

Rosemary DiCarlo amesema zaidi ya watu milioni saba wanahitaji msaada wa kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia pekee, huku takriban watu 400,000 huko Tigray wakiishi katika hali inayoshabihiana na ya baa la njaa.

Ameongeza kuwa, imepita miezi minne sasa tangu shehena kubwa ya dawa na vifaa vya afya ilipotumwa Tigray, eneo ambalo ni makazi ya watu wapatao milioni sita.

Wakazi wa Tigray

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema ripoti ya pamoja ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Ethiopia juu ya mzozo wa Tigray iliyotolewa wiki iliyopita imetoa taswira kuhusu mateso ya kutisha yanayowapata raia katika jimbo la Tigray.

Ripoti hiyo ilihitimisha kwamba kuna misingi ya kuamini kwamba pande zote katika mzozo huo - ikiwa ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia, Jeshi la Ulinzi la Eritrea, Vikosi Maalumu vya Amhara na wanamgambo washirika wao kwa upande mmoja, na wapiganaj wa Tigray  katika upande mwingine- walifanya ukiukaji wa haki za binadamu za kimataifa na sheria za wakimbizi. Pia ilieleza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huenda pia umetendeka huko Tigray.

Tags