Nov 11, 2021 08:06 UTC
  • Uchumi wa Kenya wastawi kwa asilimia 10

Uchumi wa Kenya ulistawi kwa kiwango cha asilimia 10.1 katika robo ya pili ya mwaka huu 2021.

Hayo yalisemwa jana Jumatano na Ukur Yatani, Waziri wa Fedha wa Kenya na kueleza kuwa, uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ulikuwa kwa kiwango hicho katika kipindi cha miezi mitatu hadi kufikia Juni 30, ikilinganishwa na asilimia 0.7 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Amesema miongoni mwa sekta zilizochangia kustawi uchumi wa Kenya kwa kiwango hicho cha juu ni pamoja na ya uzalishaji, elimu, uchukuzi, habari na mawasiliano. Waziri Yatani hata hivyo amesema sekta za kilimo, misitu na uvuvi hazikufanya vizuri katika kipindi hicho tajwa. 

Ukuaji wa sekta ya uzalishaji nchini Kenya uliwezeshwa na kupigwa jeki na kupanuka kwa sekta ndogo ya chakula na isiyo ya chakula katika muda huo, kwa mujibu wa Waziri Yatani.

Chumi za nchi nyingi za Afrika zastawi baada ya kupungua makali ya Corona

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha wa Kenya, sekta za uchukuzi na kuhifadhi bidhaa zimeimarika katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, baada ya kuondolewa vikwazo vya usafiri wa ndani na nje ya nchi kutokana janga la Corona, vilivyokuwepo katika robo ya pili ya mwaka jana 2020.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB ilisema uchumi wa Afrika Mashariki unatarajiwa kukua kwa asilimia 4.1 mwaka huu, likiwa ni ongezeko kutoka asilimia 0.4 mwaka jana.

Tags