Nov 12, 2021 07:53 UTC
  •  Dina Mufti
    Dina Mufti

Serikali ya Ethiopia imetangaza masharti kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano na viongozi wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF), kufuatia juhudi za kidiplomasia za kimataifa zenye lengo la kusitisha uhasama unaozidi kuongezeka huko kaskaqzini mwa nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Dina Mufti, aliwaambia waandishi wa habari jana Alkhamisi kwamba moja ya masharti ya uwezekano wa kufanyika mazungumzo ambayo amesisitiza kuwa hayajakubaliwa, ni kundi la TPLF kuondoka katika mikoa ya Amhara na Afar inayopakana na Tigray.

Dina Mufti amesema sharti la kwanza ni kusitishwa mashambulizi ya waasi wa TPLF, na pili, kondoka wapiganaji wake katika maeneo Amhara na Afar na tatu, ni kutambua uhalali wa serikali ya sasa ya Addis Ababa.

Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amesisitiza kuwa hadi sasa hakujachukuliwa uamuzi wowote juu ya uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya kusitisha vita huko Tigray.

Awali msemaji wa kundi la waasi la TPLF, Getachew Reda alikuwa amesema kuwa kujiondoa Amhara na Afar kabla ya mazungumzo kuanza ni "jambo liisilotarajiwa kabisa".

Raia walioathiriwa na vita wa eneo la Tigray

Katika siku za hivi karibuni wajumbe wa kimataifa wamezidisha juhudi za kukomesha vita na mapigano huko kaskazini mwa Ethiopia.

Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ambaye ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) alitarajiwa kuondoka Ethiopia jana Alhamisi baada ya mkutano wake wa mwisho na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed. Obasanjo alikuwa Ethiopia katika juhudi za usuluhishi na kukomesha vita huko Tigray.

Tags